Jumamosi, 23 Novemba 2013

KIBURI

Kiburi ni hali au tabia ya kukosa unyenyekevu.
Dhambi hii humwingia mtu kwa siri pasipo yeye kujua na inatenda kazi ndani yake. Mtu anapokuwa na dhambi hii hufanyika kuwa chukizo kwa Bwana, Mith 16:5.

DALILI ZA KIBURI
1. Kujihesabu kuwa yeye ni safi, Luka 18:11.
2. Kutokubali udhaifu alio nao, Mwa 3:12.
3. Hakubali kufundishwa wala kujifunza, Isaya 26:10.
4. Kuona anajua mambo yote, 1Kor 8:2.
5. Hahitaji msaada wa neno la Mungu, Mith 21:24.
6. Kutokutetemeka asikiapo neno la Mungu, Isa 66:2b.
7. Huona vigumu kumtii mwenye mamlaka, Rum 13:2.
8. Huona hawezi kujishughulisha na mambo manyonge, Rum 12:16.
9. Humzoea kiongozi wake wa kiroho, hudharau maonyo na hukosa hofu ya Mungu moyoni mwake, Mith

    10:17.
10. Hujivunia vipawa vyake, Luka 18:11.

HASARA ZA KIBURI
1. Kupata maangamivu, Mith 16:18.
2. Bwana kung'oa nyumba yake, Mith 15:25.
3. Sala zake ni chukizo, Mith 28:9.
4. Kushushwa na kuinamishwa, Mith 29:23; Lk 14:11; Mt 23:12; Yer 49:16; Isa 2:11,12.

Ijumaa, 22 Novemba 2013

DHAMBI

Dhambi ni uasi, 1Yoh 3:4; Isa 1:2; Zab 51:4; Kum 9:18.
Dhambi inaweza kutokea kwa namna mbalimbali kuanzia kwa matendo maovu, kwa makusudi mpaka kwa bahati mbaya, kwa sababu ya udhaifu, uvivu au kutokujua, Kut 32:30; Mt 5:22,28; Mit 28:13; Rum 1:29-32, 3:23; Yak 4:17.

ASILI YA DHAMBI
Kutokana na shughuli za shetani katika bustani ya Edeni inaonekana wazi kuwa dhambi ilikuwapo ulimwenguni kabla ya Adamu na Hawa hawajatenda dhambi, lakini Biblia haielezi jinsi dhambi ilivyoanza kwa asili yake bali inaeleza tu jinsi ilivyoingia kwa mwanadamu. Mwanadamu alivuka mpaka ambao Mungu alimwekea, hivyo alianguka katika dhambi. Kiburi kilikuwa kiini cha dhambi ya mwanadamu, 1Yoh 2:16; Rum 1:21-23.
Dhambi ilingia kwa sababu mwanadamu alianza kumtilia mashaka Mungu, Yak 1:14. Dhambi ilianzia moyoni mwake na tendo la kutokuamini lilikuwa matokeo yake ya lazima, Yer 17:9; Mwa 6:5.

MATOKEO YA DHAMBI
Mwanadamu alianguka chini ya hukumu ya Mungu na kuingia hali ya uadui dhidi ya:-
            1. Ulimwengu wa viumbe, Mwa 3:17-19.
            2. Wanadamu wenzake, Mwa 3:12,13; 1Yoh 3:12.
            3. Nafsi yake mwenyewe, Mwa 3:7, 11-13; Rum 7:15,19.
            4. Mungu, Mwa 3:8-10, 22-24; Rum 3:10-18.
Adhabu kuu ya dhambi ni mauti, Mwa 2:17; 3:19,24; Rum 6:23. Mauti haikuwa ya kimwili tu bali pia ya kiroho, ambayo ni kutengwa na Mungu ambaye ni asili ya chemchemi ya uzima wa kiroho, Rum 6:16,17, 5:13; 1Kor 15:56.

Jumatano, 20 Novemba 2013

UPENDO

1. Upendo ni zile hisia unazozipata wakati unapokutana na mtu unayeshabihiana naye.
2. Upendo ni kitendo cha msamaha usio na kikomo na kujali ambako huwa tabia.
3. Upendo ni mshikamano ambao hutokana na imani iliyojengeka ndani ya mtu juu ya mazuri ya mtu fulani.

                          AINA ZA UPENDO
Kuna aina nne za upendo; ambazo ni:
            1. Eros
            2. Philia
            3. Storge
            4. Agape

                 UPENDO WA EROS
Huu ni upendo wa tamaa kati ya mke na mume, Wim 3:1,4.

                 UPENDO WA PHILIA
Huu ni upendo wa kirafiki. Katika lugha ya kyunani, uupendo huu umejikita sana katika '' NIPE NIKUPE'' ambapo watu wawili wananufaishana, 1Sam 18:1-3; Yn 11:11.

                 UPENDO WA STORGE
Huu ni upendo wa kifamilia au ndugu kati ya baba, mama, kaka na  dada, Yn 11:3, 21.

                  UPENDO WA AGAPE
Huu ni upendo wa ngazi ya juu, wa Kimungu usio na ubinafsi, wenye kujitoa, usio na kikomo, usio na masharti, hauhitaji kupata chochote toka kwa yule umpendaye. Ni upendo ambao Mungu anatutarajia kuuonesha katika ulimwengu huu. Yn 3:16.

                TABIA ZA UPENDO
1. Haupungui neno lolote, unaenda popote ambako wengine hawathubutu kuenda, hutoa uhai wake, 1Kor 13:8.
2. Huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, 1Kor 13:7.
3. Haufurahii udhalimu, hufurahi pamoja na kweli, 1Kor 13:6.
4. Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, 1Kor 13:5.
5. Hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, 1Kor 13:4.

Jumanne, 19 Novemba 2013

LAANA

Ni jambo lolote linalotokea kwa kutamka, kauli, tangazo, maombi au maandishi kuelezea nia mbaya au bahati mbaya kwa mtu, familia au taifa, aidha mara moja au ya kuendelea.

AINA ZA LAANA
Kuna aina tatu za laana zinazowatesa wanadamu hapa duniani: ambazo ni:-
 1. LAANA KUTOKA KWA MUNGU
 2. LAANA YA KUJITAKIA
 3. LAANA KUTOKA KWA WATU WENGINE

 1. LAANA KUTOKA KWA MUNGU
Biblia imetamka laana wakati mtu, familia,au taifa linapotenda dhambi. Kuna pengine laana kwa kila andiko usipolitii linavyokuelekeza. Kumb 11:28; Dan 9:11; Yer 11:3; Kumb 7:25; Yos 6:18; Amu 5:23; Kumb 27:26 na Mwa 27:29.

2. LAANA YA KUJITAKIA
Lolote baya usemalo, utamkalo au ukirilo kuhusu wewe yaweza kuwa laana. Mungu amefanya maneno yetu kuwa na nguvu ya uumbaji, kama alivyoumba vitu vyote kwa kusema tu navyo vikawapo, vivyo hivyo alitoa nguvu sawa juu ya maneno yetu, Mith 18:21.

3. LAANA KUTOKA KWA WATU WENGINE
Watu waweza kutoa laana ama ana kwa ana, kwa maandishi au maombi. Mtu anayetoa laana anaweza kuwa anajulikana kwa mlaaniwa, au asiyejulikana au hata mtu fulani katika uchawi. Sababu za utamkaji wa laana zinaweza kutofautiana. Hii inaweza kuwa ni pamoja na hamu ya makusudi kumtakia mtu mabaya, inaweza kuwa ni matokeo ya ugomvi au kutokuelewana. Inaweza ikawa pia ni kwa uzembe na ujinga wa mtoa laana ambaye anadhani kuwa anatamka maneno tupu. Maombi ya kumtakia mtu mabaya huelekezwa kwa Mungu kumuomba amwadhibu mtu, familia au taifa. Njia hii ilikuwa ikitumiwa sana katika agano la kale ambapo walikuwa na maadui wanaoonekana, waliweza kumwomba Mungu ili adhibu maadui zao.

VYANZO VYA LAANA
Kuna vyanzo mbalimbali vinavyoweza kumfanya mtu apate laana; navyo ni:-

1. KURITHI
Baadhi ya matatizo yanayowapata au waliyo nayo watu katika maisha wameyarithi kutoka kwa wazazi au mababu zao. Roho hizi kutoka kwa mababu waliowatangulia kabla hawajazaliwa zaweza kuwaathiri. Kut 20:3-5; Mwa 11:30; 25:21; 29:31; 12:10; 26:1; 41:56; 12:11; 26:6,7; 27; 16:3; 30:4; 23:2; 35:19.

2. KURITHISHWA JINA
Jina lolote huambatana na roho iliyo ndani ya mwenye jina, kama mwenye jina ni au alikuwa mganga, mchawi, mgomvi, mwivi,mlevi, mwenye wivu au mvivu nawe ukarithishwa jina hilo tayari zile roho zitakuwa juu yako.

3. MAVAZI
Mavazi yana uwezo mkubwa wa kubeba roho fulani, hivyo yaliyonenewa au yaliyobeba roho chafu yana laana yanapovaliwa na mtu. Mtu huyo atatawaliwa na roho iliyo ndani ya mavazi hayo na kuwa na laana. Watu wengi wamekuwa chini ya laana mbalimbali kama vile uasherati, ukahaba, ulevi, umaskini, uzinzi kutokana na mavazi wavaayo, Mwa 38:15.

4. KUJIHUSISHA AU KUENDA KWA WAGANGA AU WACHAWI
Kuwa mganga, mchawi, kuchanjwa chale au kufanya au kufanyiwa matambiko au shughuli yoyote ile ya kiganga au kichawi ni kitendo cha kufungua mlango kwa maisha yako, biashara yako, masomo yako, ukoo wako au familia yako kuwa chini ya laana hiyo.

5. MJI AU MAHALI UNAPOISHI
Watu wengine wapo chini ya laana kwa sababu ya maeneo au miji wanayoishi,Kuna maeneo au miji ambayo ipo chini ya laana fulani mfano; utakuta mji una laana ya njaa, kila mwaka hata wakilima kwa ufanisi hawaambulii kitu, hii ni wazi kwamba kila mtoto atakayezaliwa ndani ya mji huo ataikuta na kuteswa na laana ya njaa, Mwa 12:10; 26:1; 41:56. Wakati mwingine utakuta mji au eneo fulani lina laana ya magonjwa, asilimia kubwa ya watu wanaoishi katika mji au eneo hilo wanasumbuliwa na aina fulani ya ugonjwa,
Kut 15:23; 2 Fal 2:19.

6. KIONGOZI ANAYEKUONGOZA
Maandiko yanasema ”alivyo kuhani ndivyo walivyo na watu wake” hii ina maana kwamba roho iliyo ndani ya kiongozi ndiyo iliyo ndani ya wale anaowaongoza. Kama kiongozi ana roho ya umaskini, udikteta, ufisadi, kuoa wake wengi au mla rushwa ndivyo na watu wake anaowaongoza watakuwa na roho hizo. 2 Tim1:4; Lk 22:54-61.

DALILI ZA KUWA NA LAANA
1. Kupata hisia za ajabu katika usingizi ,(jinamizi) hofu ya usiku na kupooza katika usingizi.
2. Utasa, mimba kuharibika mara kwa mara, maumivu makali ya tumbo wakati wa hedhi na siku za hedhi kubadilika badilika au damu ya hedhi kutoka mfululizo.
3. Hali ya kuwa na madeni mara kwa mara, kufilisika, kutokufanikiwa kwa chochote ukifanyacho.
4. Ugomvi katika ndoa, kutalikiana, kutengwa na familia au ukoo au ugomvi kati ya ndugu.
5. Kuachishwa kazi mara kwa mara bila sababu za msingi, kutokupata kazi  ilihali sifa zote unazo.
6. Kupoteza pesa kwa njia za ajabu au bila sababu.
7. Magonjwa ya akili, kuharibikiwa kiakili au kuhisi (kwa mfano, kuchanganyikwa au kupata kichaa).
8. Kutokuolewa au kutokuoa au kukataliwa na wachumba.
9. Kupata hasara mara kwa mara katika biashara au miradi.
10. Kutangatanga au kutokuwa na hali ya kutulia. Kuwa na hali ya kuhamahama kutoka mji fulani kwenda mji mwingine au kutoka kazi moja hadi kazi nyingine.
11. Kukata tamaa, huzuni, kukandamizwa na kujirudia rudia kwa mabaya katika maisha yako bila uwezo wa kuzuia.
12. Ukahaba, uasherati, uzinzi au kuota ndoto unafanya mapenzi na mtu ambaye si mume au mke wako.
13. Kuzorota kwa afya.
14. Kudidimia kwa mahusiano na watu, mke au mume wako.
15. Kuonewa, kufanyiwa vibaya na kunajisiwa.
16. Kujiua au vifo visivyo vya asili katika familia, ndugu kufa kabla ya wakati.

JINSI YA KUVUNJA LAANA
1. Baini jina la laana na dhambi iliyosababisha laana.
2. Tubu dhambi zako na za baba zako, mwombe Mungu aondoe haki ya laana kuwa katika maisha yako.
3. Vunja laana kwa jina la Yesu.
4. Toa/kemea mapepo yaliyokuingia kupitia laana, ukiyataja kwa majina. Baada ya kuwa mapepo yamekutoka, mwombe Mungu akuponye kimwili na kiroho.
5. Usitende dhambi tena. Unatakiwa kubadili mtazamo wako na matendo yako hata kama laana hii ililetwa juu yako na mababu.
6. Funga na kuomba, Mt 17:21.