Adui ni mtu mtu yeyote au roho yoyote iliyo kinyume na wewe yenye lengo au nia ya kuzuia maendeleo yako kimwili na kiroho.
TABIA ZA ADUI
i. Muongo, Yn 8:44c.
ii. Mjaribu, Mt 4:3; 1Thes 3:5.
iii. Mwivi, Yn 10:10.
iv. Muuaji, Yn 8:44b
v. Mpotoshaji, Mwa 3:4, 5.
vi. Mgawanyaji, Mt 26:31; Zek 13:7.
vii. Kama malaika wa nuru, 2Kor 11:14, 15.
Kila mkristo anao maadui wakuu watatu ambao ni:-
1. DUNIA
Biblia imetumia neno dunia katika nyanja tatu tofauti.
Mosi, limetumika kuzungumzia dunia ambayo Mungu kaiumba, Mdo 17:24.
Pili, linazungumzia watu, Yn 3:16.
Tatu, matumizi ya neno hili yanapatikana katika 1Yoh 2:15. Neno dunia
hapa limetumika kuelezea “mfumo wa dunia”, adui wa kila mwana wa Mungu.
Hii ndiyo fasili ya dhana ambayo tutakuwa tunatumia neno “dunia” katika
somo hili.
Shetani amepanga watu na vitu kwenye mfumo wa dunia chini
ya ubinafsi, kiburi, uloho/ulafi na tamaa za dhambi. Mfumo wa dunia wa
shetani unajumuisha burudani, biashara, elimu, dini, siasa, falme za
dunia, mashirika ya kiulimwengu na vyombo vya habari. Shetani
anawadanganya watu katika kufikiri kwamba dunia hii ndiyo jambo la pekee
linalofaa. Katika huu mfumo wa dunia shetani anaweza kuwapa watu
utajiri, milki, nguvu, umaarufu na tamaa zote za dhambi. Shetani
anawaruhusu watu kufanya mambo na kutoa maamuzi, lakini yeye mwenyewe ni
kiongozi asiyeonekana wa dunia hii, 1Yoh 5:19. Shetani anajua kuwa
hawezi akawazuia wakristo kuenda mbinguni lakini kusudi lake ni
kuwafanya wafuate mambo ya dunia. Anawataka wafikiri kama watu wa dunia
na watende mambo yale yale yafanywayo na watu wa dunia hii.
Maandiko katika 1Yoh 2:16, 17, yameyagawanya mambo ya dunia hii katika makundi matatu ambayo ni:-
i. Tamaa ya mwili (utamanifu, upenda anasa)
Ni tamaa (kutamani) ya kitu chochote kinachopendeza/furahisha/anisi
akili. Tunaporuhusu tamaa za mwili kutenda kazi isivyo halali – mambo
haya ni dhambi na ni ya kidunia.
ii. Tamaa ya macho (uyakinifu, tamaa ya vitu)
Ni tamaa/shauku ya kumiliki vile tuvionavyo. Ni tamaa binafsi
inayotokea wakati tunapoviona vitu ambavyo ni dhahiri kuwa hatuvihitaji
ila tunavitaka, ni hamu ya kumiliki, shauku ya kupata.
iii. Kiburi cha uzima (majisifu, ubinafsi)
Ni tamaa ya kuongeza faida ya mtu na kujiinua, tamaa ya kuhamakisha
sifa zake, jaribio la kufanya waa ling’are ndani yetu. Kiburi cha uzima
ni kitendo cha kujiweka juu kuwa wewe ni mtu fulani.
2. MWILI
Ni hali yetu ya ubinadamu iliyo na hali ya asili ya dhambi. Neno
“Mwili” wakati mwingine katika Biblia limetumika kuelezea “nyama.”
Lakini hapa neno “mwili” linazungumzia (utu wetu wa kale) hali yetu ya
anguko.
Biblia inatueleza kuwa tumezaliwa tukiwa na mioyo ya dhambi
na inatufanya tutende dhambi katika maisha yetu yote. Mkristo ana asili
mbili – maisha mapya (utu mpya) aliyoyapokea wakati alipomkubali Kristo
Yesu, na utu wa kale uitwao “mwili.” Utu mpya huongozwa na Roho
Mtakatifu, utu wa kale umebainishwa na tamaa za dhambi. Wakati utu mpya
unapowekwa sambamba na utu wa kale uliokengeuka ambao tulizaliwa nao
kuna vita, Gal 5:17. Mwili hushindana na mamlaka, huchoka, ni rahisi
kuendeleza mawazo ya kisasi, umeelekea kwenye kuabudu (nguvu zetu,
ujanja wetu, mawazo yetu na mwonekano wetu). Haya yote ni matamanio ya
mwili yanayohitaji kuongozwa kwa msaada wa Roho wa Mungu.
3. SHETANI
Shetani ni amiri jeshi mkuu wa mapepo anayempinga Mungu, na amejitoa
kufanya kazi ya kuwaangamiza wale walioukubali wokovu wa Bwana Yesu.
Biblia inamweleza kuwa ni mdanganyifu, mwongo, muuaji, mshitaki,
mjaribu, mwovu. Hulaghai, hupotoa, hupinga, hudanganya, hupanda magugu,
huzuia, hujaribu na kukufuru. Ni mjanja, ni mharibifu, ana injili yake,
Gal 1:6; ana kanisa lake, Ufu 2:9; ana watumishi wake, 2Kor 11:15; ana
mafundisho yake, 1Tim 4:1; ana ushirika wake, 1Kor 10:21. Shetani
anaweza fanya yote, anaweza kuzuia maisha yetu ya Kikristo. Shambulio la
shetani haliwezi kuja kwa njia ya wazi na rahisi kuonekana, huwa erevu,
pambanuzi. Shetani hutumia vivutio vya dunia na tamaa za mwili
kutujaribu na kutupata ili tutende dhambi.
NJIA AMBAZO ADUI HUZITUMIA KUWAANGUSHA WAKRISTO
1. Uchovu
Esau ni mfano amilifu wa mtu ambaye hakuchukua tahadhari kwa sababu
alikuwa amechoka. Baada ya kuwinda porini alirudi nyumbani akiwa
amechoka, akamkuta Yakobo akiandaa chakula, harufu nzuri ya makande
yaliamsha maonjo kinywani mwake, alikuwa tayari kufanya chochote ili
mradi tu ale. Aligundua kuwa mdogo wake angempa chakula kama angemuuzia
haki yake ya uzaliwa wa kwanza. Kitambo kidogo tu katika udhaifu wa
mwili, Esau akauza urithi wake kwa kande la dengu, Mwa 25:29-34.
2. Furaha
Jaribu laweza kuja katikati ya furaha yetu. Mfalme Herode ni mfano
madhubuti wa mtu aliyekamatwa katika mtego wake. Wakati wa usiku wa
sherehe yake ya kuzaliwa katika kasri lake, aliathiriwa kwa urahisi
kutokana na tamaa ya binti aliyekuwa anacheza, alikuwa akifurahia pombe,
tamaa ya kitambo tu, walakini katika saa iyo hiyo ya furaha ya hatari,
akatoa sadaka badhirifu, Mt 6:23.
3. Mashaka
Mfano mzuri ni
Petro alipojaribu kutembea juu ya maji baharini na akina mama waliokuwa
wakielekea kaburini kuupaka marhamu mwili wa Yesu, Shetani aliwafanya
waliangalie tatizo, Mt 14:29, 30; Mk 16:2.
4. Kazi nyingi, Lk 8:14; 1Yoh 5:2.
5. Mashutumu, Mwa 3:12, 13.
6. Matumizi mabaya ya ulimi, Yak 3:2, 5, 6.
7. Kukosa msimamo katika imani, Kumb 29:18; Ebr 12:15.
8. Kusinzia katika ibada, semina, mikutano au maombi, Mdo 20:9.
JINSI YA KUMPINGA
1. Uongozwe na Neno
Lifanye Neno la Mungu kuwa kiongozi wako na ukubali likutawale na uishi
kwa kila kitu lisemacho. Litakuwezesha kuenenda kwa unyoofu wa moyo na
kukulinda na aina zote za majaribu, Zab 119:9, 105.
2. Kumvaa Kristo, Rum 13:14.
3. Kutembea katika roho, Gal 5:16.
4. Kujihesabu kuwa mfu kwa dhambi, Rum 6:11.
5. Tumia jina la Yesu, Flp 2:10, 11; Kol 1:13.
6. Kuomba, Efe 6:18.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni